RC MRINDOKO AZINDUA MSIMU WA UNUNUZI WA PAMBA NA MAZAO MENGINE KWA MWAKA 2025/26
Автор: KATAVI RS
Загружено: 2025-06-09
Просмотров: 204
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameongoza sherehe ya uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa pamba na mazao mengine kwa mwaka 2025/2026, hafla iliyofanyika kwa katika Kijiji cha Kapalala na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, vyama vya ushirika, wakulima, na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo.
Katika hotuba yake, RC Mrindoko amewataka wakuu wa wilaya kuhakikisha kuwa mauzo ya mazao yote yanapitia kwenye vituo rasmi vilivyoidhinishwa na serikali pamoja na mifumo rasmi ya kibiashara. Amesisitiza kuwa utaratibu huo unasaidia kudhibiti uuzaji holela wa mazao, huku ukihakikisha wakulima wanabaki na akiba ya chakula na kuuza ziada pekee.
Ameeleza kuwa kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS), mazao ya pamba na tumbaku yanapaswa kusimamiwa kwa umakini mkubwa. Amebainisha kuwa kumekuwepo na matukio ya hujuma kutoka kwa baadhi ya viongozi wa vyama hivyo wanaokiuka taratibu za kilimo cha mkataba na kuingia mikataba isiyo rasmi na wakulima. Amewaelekeza wakuu wa wilaya kusimamia kwa karibu utekelezaji wa kilimo cha mkataba kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, ili kuwalinda wakulima dhidi ya unyonyaji unaofanywa na watu binafsi wanaotoa mikopo ya pembejeo kisha kujinufaisha na mazao ya wakulima.
Amefafanua kuwa mkoa wa Katavi umeungana na mikoa mingine katika kuanza kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuanzia na zao la ufuta katika msimu huu wa 2025/26. Ameeleza kuwa mfumo huo uliwahi kujaribiwa mwaka 2019/20 lakini ukakumbwa na changamoto zilizofanya utekelezaji usiendelee. Hata hivyo, kutokana na mafanikio yanayoonekana katika mikoa mingine, Katavi imeamua kurejea kwenye mfumo huo kwa lengo la kuhakikisha wakulima wananufaika kupitia usalama wa soko na ongezeko la thamani ya mazao yao.
Ameipongeza kampuni ya NGS Investment Company Ltd kwa kuendelea kuwa soko la uhakika la mazao ya pamba katika mkoa. Amewataka wakulima kuhakikisha wanachuma pamba kwa usafi, kuichuja vizuri na kuiwasilisha ikiwa katika ubora unaohitajika ili kuendana na mahitaji ya soko.
Aidha, amewahimiza vijana mkoani Katavi kutumia fursa ya msimu huu kwa kuwekeza kwenye kilimo, akisisitiza kuwa ni sekta yenye mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Mwakilishi kutoka Bodi ya Pamba, Bw. Bugelaha Filbert, amesema kuwa mkulima ili aweze kufaidika na kilimo chake ni lazima azalishe kwa tija, kwa maana ya kupata mavuno mengi katika eneo dogo. Amesisitiza kuwa Bodi ya Pamba inaendelea kusisitiza matumizi ya mbolea na mbegu bora sambamba na matunzo sahihi ya zao la pamba. Ameeleza kuwa kwa kufuata taratibu hizo, mkulima anaweza kuvuna hadi kilo 1,000 kwa hekari moja.
Wananchi waliohudhuria uzinduzi huo wameeleza kuridhishwa kwao na kuanza kwa msimu mpya wa ununuzi wa pamba, wakisema mfumo mpya unaotumia mizani bora na ya kisasa umeleta matumaini ya haki na uwazi katika mizani. Wameiomba serikali kuhakikisha kuwa malipo ya pamba yanafanyika kwa haraka ili kuwawezesha wakulima kupata fedha kwa wakati na kujiandaa na shughuli nyingine za kilimo na maendeleo ya kijamii.
Доступные форматы для скачивания:
Скачать видео mp4
-
Информация по загрузке: