🔴 UFAFANUZI : HATUA YA UNUNUZI UMEME ETHIOPIA | HALI YA UMEME NCHINI - KATIBU MKUU WIZARA YA NIAHATI
Автор: Bukombe Sasa OnlineTv
Загружено: 2025-03-10
Просмотров: 356
Uwezo wa uzalishaji utapanda hadi kufikia Megawati 4,031.71 ndani ya mwezi Machi 2025 baada ya kukamilika kwa mtambo wa mwisho wa Mradi wa JNHPP, kukamilika kwa mtambo huu kutafanya mitambo yote tisa (9) ya JNHPP kuwa tayari kwa uzalishaji.
Mbali na jitihada zilizofanywa kwenye uzalishaji umeme, Serikali kupitia Wizara ya Nishati
imeendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya usafirishaji umeme ili kuhakikisha; i. Umeme unafika kwa wateja ukiwa katika viwango bora (quality of power supply); ii. Upotevu wa umeme unapungua; iii. Mfumo wa Gridi unaimarika zaidi (improved system stability) na kupunguza hitilafu mbalimbali za kutoka kwa sehemu au mfumo mzima; na iv. Kiwango kikubwa cha umeme kinasafirishwa kutoka kwenye vyanzo vya uzalishaji kwenda kwa wateja waliopo pembezoni na sehemu mbalimbali za Mikoa na Wilaya.
Katika jitihada za kupunguza upotevu wa umeme, kuimarisha mifumo ya umeme pamoja na kuweza kutumia vyanzo vya umeme vyenye gharama nafuu, Nchi za Tanzania, Kenya na Zambia ziliingia makubaliano ya kujenga njia ya kusafirisha umeme (Interconnectors) inayounganisha mifumo ya Gridi ya umeme ya nchi hizo ili kupunguza gharama za uzalishaji kwa kutumia umeme wa gharama nafuu unaoweza kupatikana nchi jirani na
kupunguza matumizi ya vyanzo vya gharama kubwa.
Mradi huu ulijulikana kama ZTK (Zambia–Tanzania–Kenya) ambao mpaka sasa umekamilika kati ya Tanzania na Kenya, na unaendelea kutekelezwa kati ya Tanzania na
Zambia.
Ili kupunguza upotevu wa umeme unaotokana na kusafirisha umeme katika umbali mrefu pamoja na kuboresha ‘’stability mfumo” nchi majirani Tanzania, Kenya na Ethiopia zimeingia makubaliano ya kuuziana umeme pale ambapo nchi moja itakapokuwa na uhitaji kwa sababu za kupunguza gharama pamoja na kuimarisha mfumo wake wa Gridi ya Umeme.
Kwa kuwa vyanzo vyetu vya uzalishaji umeme vipo zaidi upande wa Kusini kwenye Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Iringa na Pwani kwa sasa, jitihada mbalimbali zinafanywa ili kuimarisha hali ya umeme upande wa kanda za Ziwa, Kaskazini Magharibi, pamoja na
Kanda ya Kaskazini.
Jitihada zinazoendelea ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa njia kubwa za kusafirishia umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma (400kV Chalinze- Dodoma) ili kupunguza upotevu wa umeme na kuimarisha mfumo wa Gridi. Vilevile njia nyingine ni kuwa na chanzo nafuu cha umeme kinachopatikana jirani na kanda hizi ambapo kwa sasa inaonekana kuusafirisha umeme wa kutoka nchi jirani ni nafuu kuliko kusafirisha umeme katika umbali mrefu ndani ya nchi.
Uendeshaji wa Masoko ya Pamoja ya Kuuziana Umeme ya Ukanda wa Mashariki mwa Afrika (Eastern Africa Power Pool [EAPP]) na Kusini mwa Afrika (Southern
African Power Pool [SAPP])
Katika kuhakikisha nchi zinazounda Ukanda wa Mashariki (EAPP) zinatumia vyanzo mbalimbali vya umeme vya bei nafuu vilivyopo kwenye ukanda huo, Nchi wanachama zimejiunga na soko la pamoja la kuuziana umeme ambapo kutokana na vyanzo vilivyopo nchi inaweza kuuza au kununua umeme wa bei nafuu kutoka kwenye nchi wanachama ili
kupunguza gharama za uzalishaji.
Kwa upande wa Kusini mwa Afrika Tanzania imejiunga na Soko la pamoja la (SAPP) ambapo tayari lilishaazishwa na linafanya kazi kwa nchi ambazo tayari miundombinu
ilishakamilika ambapo kwa sasa tunaendelea na utekelezaji wa Mradi wa TAZA ambao kukamilika kwake kutaifanya Tanzania kutumia fursa ya umeme wa unaozalishwa kwenye Bwawa la Julius Nyerere na vyanzo vingine na kuanza kuuza umeme ukanda wa kusini mwa Africa (SAPP).
Hivyo lengo kuu la kuuza au kununua umeme ni kuimarishwa kwa mifumo ya Gridi za Umeme za nchi husika pamoja na kupunguza gharama. Kwa kutumia nafasi tuliyonayo kijiografia, Tanzania itatumia nafasi ya masoko haya ya
umeme kununua na kuuza umeme wa bei nafuu kutoka ukanda wa Mashariki mwa Afrika na ukanda wa kusini mwa Afrika.
Serikali kupitia Wizara ya Nishati inaendelea kuhakikisha kunakuwepo na miundombinu
imara itakayowezesha manunuzi na mauziano ya umeme ndani ya ukanda wa EAPP pamoja na ukanda wa SAPP ili Tanzania inufaike kwa kuuza na kununua umeme lakini pia
kuingiza fedha zitokanazo na gharama za kupitishia umeme kutoka ukanda mmoja kwenda mwingine.
Доступные форматы для скачивания:
Скачать видео mp4
-
Информация по загрузке: