THRDC: Tunapochelewa kufanya maridhiano ndivyo mambo yanavyozidi kuwa mengi
Автор: WATETEZI TV
Загружено: 2025-12-05
Просмотров: 70
Katika kuelekea mwisho wa mwaka, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), unaounganisha mashirika takribani 300 nchini, umeshauri mamlaka kuanza mazungumzo ya maridhiano mapema iwezekanavyo badala ya kusubiri Tume maalum iliyoundwa kukamilisha uchunguzi.
Leo, Desemba 5, 2025, Mratibu wa THRDC Kitaifa, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema kuwa kutokana na hali ya sintofahamu iliyopo nchini, mazungumzo ya maridhiano yanapaswa kuanza haraka ili kupunguza mkanganyiko unaoendelea. Amesema kuchelewesha mchakato huo kunazidisha changamoto.
"Tunapochelewa kuingia kwenye maridhiano, kila siku matukio yanaongezeka na kufanya suala la maridhiano kuwa gumu zaidi. Tusipokuwa makini, mambo mengine yataendelea kutokea. Tunapochelewa kuingia kwenye maridhiano, mambo yanakuwa mengi zaidi," amesema Olengurumwa.
Aidha, ameshauri kuwa mchakato wa maridhiano uwe wazi na jumuishi kwa wadau wa makundi yote ya kijamii. Amesisitiza umuhimu wa watu kupewa uhuru wa kusema ukweli ili kuponya Taifa. Ametoa mfano wa Waziri wa Vijana, Joel Nnauka, ambaye kwenye ziara zake huwapa vijana nafasi ya kuzungumza kwa uwazi na ukweli.
Olengurumwa amesema si lazima mchakato huo uongozwe na viongozi wa ndani pekee; badala yake, inawezekana wakapatikana waratibu kutoka mataifa rafiki ambao wanaweza kusaidia kusimamia mchakato huo kwa lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa.
Amebainisha kuwa kwa sasa kuna hofu katika makundi mbalimbali kuhusu shughuli zao na maandalizi ya sikukuu za mwisho wa mwaka. Kwa msingi huo, ametaja umuhimu wa kupata suluhu ya haraka ili kuondoa wasiwasi huo.
Aidha amewataka viongozi wote kuzungumza kauli za kuponya na kuunganisha wananchi. Aidha, amewahimiza viongozi wa dini na wadau wengine wanaopata nafasi ya kuzungumza hadharani kuhakikisha wanazingatia hoja madhubuti na kuepuka kueneza misimamo ya kidini ambayo inaweza kuongeza mpasuko.
"Kila anayezungumza na chombo cha habari kwa sasa, ni vyema nia yake iwe kuliponya Taifa. Huu sio muda wa mashindano au kuvutana. Tusivutane kwa kuwa tutaendelea kuliumiza Taifa, tusiendelee kushupaza shingo," amesema Olengurumwa.
Hata hivyo, amesema Mtandao umesikitishwa na ukimya wa wazee waliowahi kuitumikia nchi katika nafasi mbalimbali. Amesema ukimya huo unazua maswali, ikizingatiwa uzoefu na umuhimu wao katika nyakati kama hizi. Amewataka wajitokeze na kutoa ushauri kuhusu hatua zinazoweza kusaidia nchi kutoka ilipo sasa.
Amesema kwamba kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, tayari watuhumiwa 1,146 kati ya 2,045 waliokamatwa wakati na baada ya uchaguzi, na kushtakiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo uhaini, wameachiwa huru baada ya mashtaka yao kufutwa na DPP.
Ametoa wito wa kuwaachia zaidi ya watu 800 wanaodaiwa bado kushikiliwa, pamoja na wale waliokamatwa kutokana na masuala ya kisiasa, akiwemo Tundu Lissu. Amesema kwamba mwendelezo wa jitihada hizo unaleta umoja wa kitaifa.
Aidha, ameongeza kuwa baada ya hatua za kuponya machungu kupigwa, ni muhimu kufumua mifumo ya utawala na uongozi, ikiwemo kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya ambayo ndiyo msingi mama wa nchi.
Amesisitiza kuwa kwa sasa sio wakati wa kukamata watu kiholela, kulaumiana au kuvutana. Badala yake, amesema ni muhimu kuendelea kulinda haki za binadamu na kuhakikisha ushirikishwaji mpana wakati Taifa linatafuta muafaka.
Tamko hili linakuja wakati ambao kuemeendelea kuwepo mijadala mbalimbali kwenye mitandao na vyombo vya habari kuhusu mwenendo wa hali ya kisiasa nchini Tanzania kabla na baada ya uchaguzi, ambapo matukio mbalimbali ikiwemo uvunjifu wa haki za binadamu, kauli za viongozi vikiwa sehemu kubwa ya mijadala hiyo.
Доступные форматы для скачивания:
Скачать видео mp4
-
Информация по загрузке: