IRINGA KUTOA CHANJO KWA NG’OMBE ZAIDI YA LAKI NNE KATIKA KAMPENI YA TAIFA YA CHANJO YA MIFUGO
Автор: PAMLOMO24
Загружено: 2025-11-07
Просмотров: 35
Serikali imeanza utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo kwa kipindi cha miaka mitano (2025–2029), ambapo Mkoa wa Iringa unatarajia kuchanja ng’ombe zaidi ya 400,000, mbuzi na kondoo 20,000, pamoja na kuku milioni 1.5 katika kampeni hiyo.
Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (ZVC–Iringa), Dk. Jeremiah Choga, amesema kampeni hiyo, iliyoanza Juni mwaka huu chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inalenga kudhibiti magonjwa ya mifugo na kuongeza tija katika sekta hiyo.
“Kama inavyofahamika, sekta ya mifugo hukabiliwa na magonjwa mengi. Serikali kupitia wizara imetenga fedha kwa ajili ya kutoa chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali. Kampeni hii ya miaka mitano hadi mwaka 2029 imeanza kwa kuchanja ng’ombe dhidi ya homa ya mapafu, huku maeneo mengine yakihusisha mbuzi, kondoo na kuku,” alisema Dk. Choga.
Aliongeza kuwa serikali imetenga shilingi bilioni 216 kwa ajili ya utekelezaji wa kampeni hiyo, ambayo pia inahusisha kuvalisha mifugo heleni za utambuzi ili kudhibiti wizi na kuboresha usimamizi wa takwimu za sekta hiyo.
“Faida za kampeni hii ni pamoja na kujua idadi halisi ya mifugo nchini, kupunguza magonjwa, kuboresha afya ya mifugo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya mifugo,” alifafanua.
Katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, zaidi ya ng’ombe 8,000 sawa na asilimia 88 ya lengo tayari wamepatiwa chanjo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupambana na magonjwa ya mifugo.
Dk. Aldonis Ulimboka, Daktari wa Wanyama wa Halmashauri hiyo, alisema kati ya ng’ombe 10,000 waliolengwa, wengi wao tayari wamechanjwa na kutambuliwa kupitia mfumo mpya wa utambuzi wa mifugo.
Wafugaji mkoani humo wamepongeza juhudi za serikali, wakisema kampeni hiyo itaboresha afya ya mifugo na kuongeza uzalishaji.
Gwamaka Mwakang’ata, mfugaji kutoka Kata ya Changarawe, alisema chanjo hizo zitasaidia kupunguza vifo vya mifugo na kuongeza kipato cha wafugaji.
“Tunamshukuru serikali kwa kugharamia chanjo hizi. Zimeleta faraja kwa wafugaji na tija katika uzalishaji,” alisema Mwakang’ata.
Naye Michael Nyalusi kutoka mtaa wa Ngome alisema kampeni hiyo imepunguza kwa kiwango kikubwa magonjwa ya mifugo yaliyokuwa yakiwaathiri wafugaji kwa muda mrefu.
“Hali imebadilika sana. Zamani tulipoteza mifugo mingi kutokana na magonjwa yanayozuilika, lakini sasa tumeona matokeo chanya,” alisema.
________________________________________
Доступные форматы для скачивания:
Скачать видео mp4
-
Информация по загрузке: